Unknown
Shalom,
Tunajua unataka uwe na uchumi mzuri. Hii
ni kwa mwanadamu yeyote bila kujali mahali alipo,awe anafanya kazi au
hata kama hafanyi kazi.
Kuanzia leo na siku kadhaa
zitakazofuata,tutajitahidi kukushirikisha misingi kadhaa iliyomo katika
biblia,ambayo tunaamini itakusaidia uwe na uchumi mzuri. Msingi wa
kwanza ni huu:Badilika unavyoamini juu ya uchumi,utabadilika unvyosema
juu ya uchumi,na hali yako ya uchumi itabadilika vivyo hivyo.
Tunaamini ya kuwa; mtu akibadilika anavyoamini atabadilika pia anavyosema;na hali yake ya maisha itabadilika vivyo hivyo.
Jambo hili tunalipata tunaposoma kitabu cha Mithali 23:7 ya kuwa; “Maana aonavyo nafsini mwake,ndivyo alivyo.”
Tafsiri nyingine ya mstari huu inasema;”maana awazavyo nafsini mwake
ndivyo alivyo.” Tasfiri nyingine ya mstari huu inasema;”maana aaminivyo
nafsini mwake,ndivyo alivyo.” Mstari huu unataka tujue ya kuwa maisha ya
mtu alivyo ni matokeo ya awazavyo au aaminivyo au afikirivyo(mindset),
nafsini mwake.
Ulivyo kimaisha kwa nje ni matokeo ya
msimamo wako wa kimawazo ndani yako. Kwa ulivyo kiuchumi,ni matokeo ya
msimamo wako kimawazo(mindset),ulionao ndani yako juu ya uchumi.
Wapelelezi 10 walileta habari mbaya
walipotoka kuipeleleza Kaanani,kwa vile waliamini mioyoni mwao ya kuwa
“majitu” waliyoyakuta Kaanani yalikuwa kikwazo na pingamizi
kwao.Wapelelezi wawili (Yoshua na Kalebu),waliona hayo “majitu” pia
lakini mioyoni mwao waliamini tofauti. hawakuyaona majitu kama kikwazo
bali waliyaona kama fursa kwao ya kutatua tatizo hilo ili waweze kula.
Soma habari hii katika kitabu cha hesabu 13:32,33 na Hesabu 14:9,28
Matokeo ya tofauti hizo kuwaza na kuamini,kuliamua hatma ya baadaye ya
uchumi na maisha yao.Wapelelezi 10 waliishia kulalamika na kushindwa
kwenda Kaanani. Na wale wawili (Yoshua na Kalebu) waliweza kwenda
Kaanani na wakawa na maisha mazuri.
Wazo tunalokufikirisha siku hii ya leo
ni kwamba;Usiyaone matatizo ya kiuchumi yanayokuzunguka kama
kikwazo,bali yaone fursa ya kuyatatua ili iwe njia mojawapo ya kuongeza
kipato chako. Kumbuka wanaolalamika wanapoona matatizo,wanajipofusha
fikra szao wasiona fursa za kimaendeleo katika matatizo hayo.
Mungu awabariki.
Christopher & Diana Mwakasege(Mana Ministry)