TOFAUTI YA ZAKA NA DHABIHU

Mwl. Christopher Mwakasege

Kutokutoa zaka na dhabihu ni kumwibia Mungu. Mtu aliye mkristo asipotoa zaka na dhabihu anaitwa mwizi. Kuna wakristo ambao ni wezi lakini wao hawajui yakuwa ni wezi. Wamemwibia Mungu zaka na dhabihu. Mungu anasema hivi: 

             “Je! mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia ZAKA na DHABIHU” (Malaki 3:8) 

            Kati ya amri tulizopewa na Mungu ni kwamba tusiibe. Kuiba ni dhambi. Na dhambi ina adhabu yake. Popote palipo na dhambi, laana hutokeza. Kwa wale wanaomwibia Mungu kwa kutokutoa zaka na dhabihu, wamefunikwa na laana. Ndiyo maana Mungu alisema hivi:

                “….. Mmeniibia Zaka na Dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana;   maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote  (Malaki 3:8b, 9).
            Laana maana yake ni kutokufanikiwa, kutofaulu, kutokustawi, kukosa furaha, kukosa amani, na kukosa mwelekeo sahihi. Ni wazi kuwa wakristo wengi hawana furaha, hawana amani na hawafanikiwi katika maisha yao ya kila siku, kwa sababu hawamtolei Mungu zaka na dhabihu. 

            Unapokosa kumtolea Mungu ili ujenzi wa nyumba yake – kanisa uendelee, Hagai 1:6 anatuambia Mungu anasema hivi;

            “Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka”. 

Zaka ni kitu gani?
              Zaka ni fungu la kumi la pato lako. Hebu isome na kuitafakari mistari ifuatayo;
             “Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana, ni takatifu kwa Bwana ….Tena zaka yote ya ng’ombe, au ya kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; SEHEMU YA KUMI watakuwa ni watakatifu kwa Bwana” (Mambo ya Walawi 27:30 –32).

            “…Toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako,  akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo”(Kumbukumbu la Torati 14:28-29). 

            Zaka ni fungu la kumi la pato toka mshahara wako ofisini, shambani au kwenye mifugo. Tena zaka hii ni ya Bwana na ni Takatifu.
                    Mtu asipoitoa zaka hii anamwibia Mungu. Zaka si yako hustahili kukaa nayo wala kuitumia nje ya utaratibu wa Mungu. 


                    Lakini Malaki 3:10a anasema; “Leteni zaka KAMILI ….” Maana yake nini maneno haya? Maana yake ni hii; ikiwa kwa mfano mshahara wako kwa mwezi ni shilingi 2,000/= ( kabla ya makato) – fungu la kumi au zaka unayotakiwa kutoa ni shilingi 200/= ambayo ndiyo zaka kamili ya mshahara wako. Ukileta pungufu yake hiyo si zaka kamili.
                         Tena kwa mfano umevuna magunia 10 ya mahindi toka shambani mwako – zaka kamili unayotakiwa kutoa ni gunia moja bila kupungua. Kumbuka mzaliwa wa kwanza wa mifugo yako ni wa Bwana. 

                        Unaweza ukasema habari za kutoa zaka ni za agano la kale na siyo za agano jipya.
            Waebrania 7:5-10 inatuambia wazi ya kuwa Ibrahimu alitoa fungu la kumi. Kama Ibrahimu alitoa sehemu ya kumi, Je! si zaidi sana kwetu sisi tulio uzao wake kwa imani ndani yake Kristo? Maana imeandikwa hivi;

            “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu na warithi sawasawa na ahadi” (Wagalitia 3:29). Soma pia Wagalitia 3:13,14). 

Dhabihu ni kitu gani?
            Dhabihu ni matoleo yanayotolewa baada ya kutoa sehemu ya kumi ya pato lako. Kwa mfano, kama mshahara wako kwa mwezi ni shilingi 2,000/=, basi sehemu ya kumi (zaka) ni shilingi 200/=. Kiasi cho chote utakachotoa ju ya shilingi 200/= ndiyo matoleo yako. Kwa mfano ukitoa shilingi 210/= toka kwenye mshahara wako wa shilingi 2000/=, Basi, shilingi 200/= ni zaka; na shilingi 10/= ni dhabihu au matoleo au sadaka ya kawaida.
            Kiasi utakachotoa katika dhabihu/matoleo, ndicho kitakachokuwa kipimo kitakachoweka kiwango chako cha kupokea. Imeandikwa hivi:

            “Lakini nasema neno hili, APANDAYE HABA ATAVUNA HABA; APANDAYE KWA UKARIMU ATAVUNA KWA UKARIMU. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, MKIWA NA RIZIKI ZA  KILA NAMNASIKUZOTE,mpatekuzidisanakatikakilatendojema;kamailivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye ATAYAONGEZA MAZAO YA HAKI YENU, MKITAJIRISHWA KATIKA VITU VYOTE MPATE KUWA NA UKARIMU WOTE; umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. 

Maana utumishi wa huduma hii HAUWATIMIZII WATAKATIFU RIZIKI WALIZOPUNGUKIWA TU, Bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu; kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, WANAMTUKUZA MUNGU kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote” (2Wakorintho 9:6-13)

            Soma tena mistari hiyo hapo juu, lakini sasa tafakari zaidi maneno niliyoyaandika kwa herufi kubwa. Utaona kuwa usipokuwa mwaminifu katika utoaji, wewe mwenyewe unakosa kufanikiwa, na pia unamkosesha Mungu shukrani na utukufu ambao angepata kwa utoaji wako. 

Zaka na dhabihu zitolewe wapi?
            Hili jambo linahitaji uongozi wa Roho Mtakatifu, ili upate ufahamu Mungu anataka upeleke wapi zaka na matoleo uliyo nayo.
            Hili ni muhimu kwa kuwa Biblia inazungumza juu ya kupeleka kanisani (Malaki 3:10-11), kwa watakatifu (2Wakorintho 9:12), kwa maskini (2Wakorintho 9:8-9), kwa watumishi wa Mungu (1Wafalme 17:10-24; 1Wakorintho 9:7-14); kwa wajane, - na kadhalika.
                Muombe Mungu akuongoze mahali pa kupeleka. Amani ya Kristo na iamue moyoni mwako. 

Baraka Tele!
            Kuna baraka tele za mafanikio kwa mkristo aliye mwaminifu katika kumtolea Mungu zaka na matoleo. 

            Katika Malaki 3:10 imeandikwa hivi; “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo (YA UTOAJI) asema Bwana wa Majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na KUWAMWAGIENI BARAKA, HATA ISIWEPO NAFASI YA KUTOSHA AU LA”
.
             Je! umewahi kukutana na mkristo ambaye anashuhudia kuwa Mungu amempa baraka nyingi hata HANA MAHALI PA KUZIWEKA? Ni wazi kuwa ahadi hii haijatimia kwa kuwa hatujawa watendaji na Neno kikamilifu katika utoaji. 

              Soma mistari hii hapa chini uone baraka zingine zinazotokana na utoaji; “Azaria Kuhani Mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza kuleta matoleo nyumbani kwa Bwana, tumekula na KUSHIBA NA KUSAZA TELE; kwa kuwa Bwana amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa. Ndiko Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa Bwana; wakavitengeneza. Wakayaingiza MATOLEO na ZAKA na vitu vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu ….” (2Mambo ya Nyakati 31:10-12). 

            Kwa nini wakristo wengine wanapungukiwa vyakula, wakati tuna nafasi ya kumruhusu Mungu kutubariki kwa vyakula tele? Mpe Mungu nafasi ya kukubariki kwa kumtolea zaka na matoleo! 

Anza Sasa!
             Nakushauri ya kuwa kama ulikuwa hutoi sehemu ya kumi au zaka pamoja na  matoleo ya kutosha – anza sasa.
             Jambo la kwanza, kumbuka kutubu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo kwa kuwa ulimwibia zaka na dhabihu kwa kutokumtolea.
            Halafu mwombe Mungu akuwezeshe kusimama katika uaminifu wa kumtolea zaka na dhabihu ili apate nafasi ya kukubariki zaidi kama tulivyoona, na kama alivyoahidi.

Mwl Christopher Mwakasege.

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More